Wakati uliopita
tuliangalia namna ambavyo Akili ikitumika ipasavyo inaweza ikamfanya mtu
akatumikiwa na wenye nguvu nyingi za Mwilini. Tuliona namna ambavyo Lionel
Messi huwatesa Wachezaji wengi wa timu pinzani kwa sababu ya kiwango kikubwa
cha uwekezaji aliyoufanya kwenye Akili zake. Ikiwa nawe unahitaji kufanikiwa
kama Messi kwenye eneo lo lote lile, huna budi kuwekeza kwenye Akili yako –
unao uwezo mkubwa sana wa kuifanya Akili yako ilale au iamke, ikimbie au itembee,
isinyae au istawi na kuchanua, izae au iwe tasa.
Kama ulipitwa na sehemu
ya kwanza ya Siri za Mafanikio - Tumia Akili zako ipasavyo, huna budi kujifunza
kwanza kupitia hii link yenye maandishi ya bluu hapa chini ili twende sambamba;
Sasa, siku hii ya leo
ninawiwa kukuletea siri ya pili ya mafanikio iliyotumiwa na akina Bakresa, Mo
Dewji, Reginald Mengi, Shabiby, Maznat, Oprah, Dangote, Masanja Mkandamizaji,
na wengine wengi unaowajua na kuwasikia. Ikiwa wao walio binadamu kama sisi waliweza
kufanikiwa, hata nasi inawezekana kwa kutumia siri walizozitumia wao. Ili nisikuchoshe,
siri yenyewe hii hapa chini;
(02) FANYA
KAZI
KWA BIDII.
Mojawapo ya majanga
makubwa yanayoitesa Afrika ni Uvivu unaoambatana na ufanyaji wa kazi kimazoea –
kufanya kidhaifu kama akina fulani na kutegemea matokeo makubwa. Vijana wengi
wa kitanzania, au wa kiafrika wanapenda sana kuweka bidii ndogo sana kwenye
jambo na kutegemea Mavuno makubwa. Matokeo yanapokuwa madogo, wanaanza kusema
ya kwamba Wamelogwa, au wanafuatiliwa na roho za kiukoo za Umaskini. Na ndio
maana hata waonapo wengine wamefanikiwa wanaanza kuwashutumu ya kwamba
wanatumia Mazingaombwe, Freemason, Mazindiko na Kafara. Nadhani nawe ni shahidi
mwaminifu katika hili.
Baada ya wajasiriamali wa
nje kuona vijana wengi wa kiafrika hawapendi kufanya jambo lo lote lile kwa
bidii ili kuwa na hali nzuri za kiuchumi na kimaisha; wakaja na kampeni za
kubeti kwa pesa kidogo ili kuvuna mamilioni, wakaja na kampeni za biashara ya
mtandao – network marketing, ya kuwaaminisha ya kwamba wanaweza kuwa mamilionea
wapya bila kufanya kazi kwa bidii – wenyewe ni kulala tu na kufanya mambo yao
mengine huku pesa zikiendelea kuingia na kujaa kwenye akaunti zao za kwenye
simu na benki. Mamia ya vijana wakatumia fedha zao za akiba kujiingiza huko
kichwa kichwa, baada ya muda wakaanza kurudi na misemo ya ‘Ningejua! Ningejua’
na kuchukia michezo ya kubahatisha. Ingawa wengine bado wanajiingiza huko.
Ndugu msomaji,
“mtu ye yote Yule
ambaye atakuletea FURSA mpya ya kukufanikisha kifedha bila kufanya kazi kwa
bidii, mkimbie na umwogope kama dhambi. Hakuna uhuru wa kiuchumi usiomwitaji
mtu kufanya kazi kwa bidii, kama huamini kawaulize matajiri wote unaowafahamu.” – Lamax
– utawakuta wanafanya kazi kwa bidii kuliko
maskini walio wengi. Kufanya kwao kazi kwa bidii hakumaanishi ya kwamba
wanauchu sana na Utajiri usiokuwa na mwisho, ila kwa sababu kazi ni Utu. Kuishi
bila kufanya kazi ni kufa bila kujielewa.
Ulishawahi kujiuliza ni
kwa nini Walokole wengi wana hali ngumu za kiuchumi licha ya kusema ya kwamba
Mungu wao anamiliki fedha na dhahabu zote, naye alikwisha kuwabariki!! Ni kwa
sababu ya kutokufanya KAZI kwa BIDII. Wengi wao wanadhani MAOMBI ndio njia ya
MKATO ya kuwafikisha kwenye Uhuru wa KIFEDHA. Kumbe sivyo!
Mungu hawezi
akamfanikisha mtu ye yote Yule asiyefanya kazi kwa bidii – Yeye huliangalia
neno lake apate kulitimiza. Anasema ya kwamba, ‘Atendaye mambo kwa Mkono mlegevu
huwa Maskini; Bali mkono wake aliye na BIDII HUTAJIRISHA.’
Tena anaongezea kwa
kusema, ‘Akusanyaye wakati wa Hari ni mwana mwenye Hekima; Bali asinziaye wakati
wa Mavuno ni mwana mwenye Kuaibisha.’
Ndugu msomaji; unataka kuwa
mwandishi kama Emmanuel Makwaya au Lackson Tungaraza, Mwalimu kama Dickson
Kabigumila au Raphael Lyela, Mwamasishaji kama Joel Nanauka au Paul Mashauri,
Mchekeshaji kama Joti au Masanja, Mwimbaji kama Angel Benard au Ambwene,
Mwanasoka kama Ronaldo au Samatta, Kiongozi kama Nyerere au Nelson Mandera,
Mwanasiasa kama Tundu Lissu au Zitto Kabwe, Mhubiri kama Reginald Bonke au Fred
Msungu, na wengine wengi?
Siri mojawapo ni KUFANYA KAZI
YAKO KWA BIDII.
Kama ni kuimba, imba kwa
bidii. Kama ni kuandika, andika kwa bidii. Kama ni kucheza mpira, cheza kwa
bidii. Kama ni kusoma, soma kwa bidii. Unajua ni kwa nini ufanye hivyo? Kwa sababu
ndio siri itakayokuketisha na Wakuu.
Mwenye Hekima mmoja aitwaye Sulemani alisema ya kwamba,
‘LO
LOTE MKONO WAKO UTAKALOLIPATA KULIFANYA, ULIFANYE KWA NGUVU ZAKO
– KWA BIDII’
Tukutane baadae kwa mwendelezo wa Somo la SIRI ZA MAFANIKIO. Hata hiyo
Siri ya kufanya kazi kwa Bidii sio kwamba nimegusia kila kitu, ila nimekupatia
maeneo ya Msingi zaidi.
Unaweza kujipatia VITABU
vya Lackson Tungaraza, aidha cha ‘SITARUDI
NYUMA TENA’ au cha ‘MWANACHUO DIARY’- Bofya hapa chini kujua kwa Undani kitabu cha Mwanachuo Diary;
Pia unaweza kujipatia
Somo ambalo liko kwenye mfumo wa Sauti (audio) liitwalo ‘KIJANA NA UMAARUFU –
Kuna Raha ya Kuwa Maarufu’ – utaweza kulipata kwa kutumiwa Mtandaoni.
Mawasiliano ya kupata Vitabu na Somo la Audio:
0764-793105 (ipo pia WhatsApp)
Zaidi: JIFUNZE
YouTube ( www.YouTube.com/c/lacksontungaraza
),
Facebook Page ( @tungarazalackson )
0 comments:
Post a Comment