Thursday, January 14, 2016


JULIUS K. NYERERE


Tunayo mengi ya kujifunza na kujivunia kwa mwalimu nyerere, Mwasisi na Baba wa taifa la Tanzania.
MWL. JK NYERERE 

AKIWA NA RAIS WA AWAMU YA NNE, DR. JAKAYA MRISHO KIKWETE, 
MZEE WA ARI MPYA, NGUVU MPYA NA KASI  MPYA

Kuzaliwa na Malezi
Julius Kambarage Nyerere alizaliwa April 12/1922 katika ardhi ya Tanganyika, na alifariki tarehe 14/10/1999 mjini wa London Uingereza. Alizaliwa katika kijiji cha Butiama, karibu na pwani ya mashariki ya Ziwa la Victoria. Nyerere alikuwa mmoja wa watoto ishirini na sita wa baba yake, Nyerere Burito. Baba yake alikuwa kiongozi wa kabila la Zanaki. Pia baba yake alikuwa na fedha nyingi lakini hakuwa na  elimu kubwa.

Wakati wa utoto wake, Julius Nyerere alichunga mifugo na alikuwa na maisha ya kawaida. Nyerere alikuwa mfuasi wa dini ya Katholiki, alihudhuria misa mara kwa mara. Watu wanasema alipenda sana kucheza na kufanya mizaha. Pia alichonga meno yake ya mbele na msumeno kuonyesha utamaduni wa kabila lake.

Elimu
Julius Nyerere alijiunga na Shule ya Msingi ya Serikali katika mji wa Musoma wakati alipokuwa na miaka kumi na miwili. Alimaliza masomo ya miaka minne kwa miaka mitatu kwa sababu alikuwa na akili sana, alienda kusoma Shule ya Upili ya Serikali ya Tabora. Huko, alipata udhamini wa kwenda Chuo Kikuu cha Makerere. Ni muhimu kujua wakati alipopata udhamini huo, Makerere kilikuwa Chuo Kikuu cha pekee katika Afrika ya Mashariki. Alipata shahada yake hapo.

Baada ya chuo kikuu, Nyerere alirudi Tanganyika na alifanya kazi katika Shule ya Upili ya St. Mary katika mji wa Tabora. Shule ya St. Mary, ilikuwa shule ya katoliki. Huko, alifundisha masomo ya Biolojia na Kiingereza. Mwaka 1949, alipata udhamini wa kwenda kusoma katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, hivyo akawa Mtanzania wa kwanza kusoma chuo kikuu nchini Wingereza na Mtanzania wa pili kupata digrii nje ya Afrika.

Katika chuo kikuu cha Edinburgh, Nyerere alipata Shahada ya juu ya Sanaa katika Historia na Uchumi, mwaka 1952. Akiwa Edinburgh, alisoma mkondo wa kufikiri unaoitwa “Fabian.” Mkondo wa “Fabian”, ulijumuisha kundi la wataalamu wa Ujamaa wa Uingereza. Azimio la “Fabian” ni kuendeleza mawazo ya kijamaa. Kwa sababu alijifunza mawazo ya “Fabian,” alianza kufikiri mabadiliko mazuri sana yangepatikana ikiwa angeweza kuunganisha ujamaa na maisha ya Afrika. Wakati wa maisha yake, Nyerere aliitwa “mwalimu” kwa sababu ya kazi zake za uelimishaji.

Ndoa na Familia
Kabla ya maisha yake ya kuwa mwanasiasa, alioa mwanamke aliyeitwa Maria Magige. Maria alitoka kabila tofauti. Wanahistoria walisema alioa mwanamke wa kabila lingine kuonyesha dunia,ilikuwa muhimu sana kusahau tofauti baina ya makabila na kuwa wamoja.

Mchango Katika Jamii
Mchango mkuu wa Nyerere katika jamii ni kazi aliyofanyia serikali. Lakini kwanza tusisahau kwamba, Nyerere alikuwa mwalimu wa historia, Kiingereza, na Kiswahili. Hivyo alianza shughuli za kisiasa alipokianzisha chama cha TANU (Tanganyika African National Union) kupigania uhuru kwa nchi za Tanganyika. Ndani ya mwaka mmoja tu, TANU ilikuwa na watu wengi wapya na ilikuwa ikiongoza  miradi ya kisiasa Tanganyika. Kwa sababu Nyerere alianza kujihusisha na siasa, hivyo alihitaji kuamua baina ya maisha ya uwalimu au ya uwanasiasa. Alijiuzulu kutoka kufundisha, na kuwa Mwanasiasa .

Alisafiri ndani ya Tanganyika kuzungumza na watu wengi na viongozi tofauti, kujaribu kupata msaada katika harakati za uhuru wa Tanganyika. Katika mwaka 1954, alifaulu kuunganisha jamii mbalimbali kitaifa pamoja kusaidia harakati za uhuru.  Nyerere alikuwa na ujasiri wakuzungumza, ujasiriuliomsaidia alipozungumza na UN (Umoja wa Mataifa) kuhusu uhuru wa Tanganyika. Mwaka 1958, aljiunga na Colonial Legislative. Tarehe 9/12/1961, Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika baaada ya kupata Uhuru.
UHURU WA TANGANYIKA, NYERERE NA WANANCHI WAKISHEREKEA 

 Baada ya mwaka mmoja yaani mwaka 1962, Nyerere alishinda uchaguzi na kuwa rais wa Tanganyika. Pia  ni muhimu kujua kwamba Nyerere alifaulu kuunganisha kisiwa cha Zanzibar na Tanganyika  pamoja kuunda nchi ya Tanzania katika mwaka 1964, baada ya mapigano huko Zanzibar yaliyomaliza utawala wa Jamshid bin Abdullah, kiongozi wa Zanzibar.
KUUNDWA KWA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Nyerere aliendelea kuwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania mpaka mwaka1985. Akiwa Rais, Nyerere alikumbwa na matatizo mengi kwa sababu mwaka 1960 Tanzania ilikuwa nchi maskini sana ukilinganisha na nchi zingine duniani, hivyo kuwa na deni kubwa sana na pia kulikuwepo na mfumuko mkubwa wa bei. Katika kusaidia nchi yake, Nyerere aliamua kujaribu ujamaa na maisha ya pamoja vijijini, na utaifishaji. Aliandika dhana zake katika Azimio la Arusha la Mwaka 1967. Watu walihimizwa kuishi na kufanya kazi pamoja katika vijiji vilivyokusudiwa kusambaza desturi ya utamaduni wa Tanzania na kuunda umoja.

JK. NYERERE AKIWA KWENYE BAISKELI YAKE,
 HAKUPENDA KUJILIMBIKIZIA MALI
ALIKUWA MTU WA WATU
Baada ya shughuli zake za urais, Nyerere aliendelea kusaidia jamii yake. Alikuwa mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM).  Miaka michache baadae, aliacha shughuli za kisiasa kwa sababu ya umri wake. Alirudi kupumzika katika kijiji chake huko Butiama alipozaliwa. Tarehe 14/10/1999, alifariki mjini London alipokuwa amelazwa kwa matatizo ya kiafya.  Je, wewe kama Mtanzania unalipi la kusema juu ya Mwasisi wa taifa letu Mwl. JK Nyerere?
MWL. JK NYERERE AKIWA AKITA UBORA WAKE, 
A MAN OF VISIONS 
Toa maoni yako hapa na pia washirikishe wengine (share)

Imeandaliwa na rafiki yako mpendwa, Mr. Lackson Tungaraza
Blogger & Motivator
0764793105 (whatsapp/sms/call).

0 comments:

Post a Comment

MAKUNDI YA MASOMO YETU

CHAGUA MASOMO HAPA

Powered by Blogger.

ZILIZOSOMWA ZAIDI